|
MWANAMUZIKI nguli wa muziki wa reggae kutoka Afrika Kusini, Lucky Dube, alipata kuimba katika moja ya nyimbo zake kuwa, ‘If you follow politician, you will never come far,’ kwamba ukiwasikiliza na kuwafuata wanasiasa hautafika mbali. Watakuacha solemba tu. Kwa maana ya kwamba wanasiasa si watu wa kuaminika sana, wakati wote.
Kwa mfuatiliaji wa masuala ya siasa, sehemu yoyote hapa duniani, achilia mbali Tanzania, anaweza kuwa na mifano mingi tu, kuweza kuelezea na kulithibitisha hili. Wazo hili linaweza kuungwa mkono na hoja nyingine kwamba katika siasa hakuna rafiki wala adui wa kudumu.
Adui yako mkubwa leo anaweza kuwa rafiki yako mkubwa kesho na kinyume chake. Ndiyo maana mtu hapaswi kushangaa leo Wamarekani wakimsaka rafiki na kipenzi chao hapo zamani – Osama Bin Laden. Haishangazi kusikia kuwa Jonas Savimbi aliuawa baada tu ya waliokuwa wakimpa kiburi, kumsaliti kwa serikali ya Angola, si wengine nao ni hao hao Marekani.
Mlolongo unaweza kuwa mrefu, usishangae pia unapomuona ghafla, Muammar Gaddafi, rais aliyekuwa akihesabika kuwa mmoja wa adui wa nchi ya Marekani na washirika wake wa Ulaya, sasa ni mtu wao wa karibu.
Hiyo ndiyo siasa. Lakini pia hayo ni ya Musa (ughaibuni), ya Firauni (hapa nyumbani), pia yanaweza kukumbukwa na kuonekana. Wapo akina Leo Lekamwa na Augustine Mrema. Tunaweza kuwakumbuka watu kama Masumbuko Lamwai na Tambwe Hiza, tukiwataja kwa uchache tu. Historia inaonesha hivyo, haijafutika.
Halafu kuna hili na Zanzibar kuwa ni nchi au la, nalo limetufikisha katika uhalisia wa wanasiasa wetu na siasa kwa jumla. Suala limezua suala, kila mwenye uwezo wa kusema ameshasema na kunukuliwa na vyombo vya habari.
Mara nyingi kwa watu wafuatiliaji wa ‘mtifuko’ wa kisiasa Tanzania, hasa unapohusisha masuala ya Muungano kuna watu ambao hawawezi kujiuzia kulisema.
Haliwezi kupita jambo la nafasi ya Zanzibar katika Tanzania usiwasikie watu kama akina Raza, Maalim Seif Sharif Hamad na wengine (kwa siku za hivi karibuni wanavuma pia akina Shamuhuna.
Wote waliotarajiwa kupaza sauti zao katika suala hilo, ambalo chimbuko lake ni kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati akitoa hotuba ya majumuisho ya Ofisi yake, wameshafanya hivyo.
Hilo limesababisha kuwa na ‘Muungano usio rasmi’ kati ya mahasimu wakubwa wa siasa za Zanzibar – CCM na CUF. Hiyo ndio siasa.
Jamaa sasa wanaonekana kuwa ni kitu kimoja, mtu akihisi kuwa kwa sasa hawa jamaa wanaweza hata wakakutana kwa siri na kupanga mikakati ya kuibuka na hoja za pamoja, hata kama wasipotaka kuonesha hivyo hadharani, atakuwa hakosei.
Kwamba wahafidhina na wanamageuzi wanaweza kukaa meza moja kwa suala hili na mwisho wa siku wakaongea lugha moja, ni suala ambalo linaweza kusubiri muda tu kwa jinsi wanasiasa wetu wanavyoendesha mambo kwa kubahatisha, bila kuwa na mpangilio.
Halafu, wanasiasa walivyo watu wa ajabu wenye kutaka kulazimisha kidole cha shahada kiwe sawa na cha kati kwa urefu na ukubwa. Katika hili la Zanzibar yameingizwa mambo mengi ambayo hapo awali hayakufikiriwa.
Wahusika (wanasiasa) wote wanaorusha hoja zao, vijembe vyao, jeuri yao na kupima mbavu zao katika ulingo wa siasa, hasa wakijaribu kupinga hoja ya Pinda, kwa hoja za nguvu (badala ya nguvu ya hoja). Hawataki kuwaeleza wasikilizaji wao kuwa kati ya dola, nchi, taifa kipi hasa kinagomba hapa.
Mwanasiasa yeyote makini hasa kutoka chama makini chenye kuwa na washauri wa masuala ya sheria na katiba, bila shaka angelitazamiwa kuja na hoja iliyotokana na tafakuri jadidi.
Angechambua hoja, kupitia misingi yote na hatimaye kufikia hitimisho murua, lenye mantiki na linaloeleweka akiwaacha watu wakiwa wameelewa.
Kama mtu wa kawaida hawaelezwi masuala ya namna hii kwa ufasaha bila kuangalia mtaji wa kisiasa, tunaweza kuwa na uhakika kabisa hata tuliowasikia majuzi wakiwa wamehamasika (au kuhamasishwa?) kuandamana eti kumpinga Waziri Mkuu, wakiulizwa mmoja mmoja nini hasa kilichowafanya kutaka kubeba mabango, wachache mno watakaoweza kukuambia kitu chenye mantiki kuonesha kuwa wanajua wanachokitaka.
Wanasiasa kama akina Raza, Maalim Seif au Shamuhuna (kuwataja kwa uchache), ndio wenye kuweza kuwafikia kwa urahisi zaidi wananchi wao, kuliko akina Profesa Shivji, Haroub Athuman au Mwesiga Baregu na wataalamu wengine ambao wamekuwa wakijaribu kuzielezea zana zote hizo za taifa, nchi au dola.
Wengine wanasema kuwa wanapanga kuzunguka kote visiwani eti kuzidi kuwahamasisha Wazanzibari waendelee kusimama kidete kutetea ‘nchi’ yao.
Lakini hamadi ni iliyo kibindoni, wanatafuta kuungwa mkono katika upande ambao tayari wameshachukua msimamo bila kujali kama utakuwa na maslahi kwa wananchi wote.
Unapomsikia kiongozi wa serikali, akiwa pia na kofia ya uanasiasa, anatoa kauli kumjibu mkubwa wake kuwa hizi si zama za kutishana na kubembelezana kuhusu Muungano, anafaa kutazamwa kwa macho makini.
Kwani wakati Pinda akiibua hoja ile alimtisha mtu? Mbona alipata kurudia kwa masikitiko akisema alimaanisha nini. Lakini hawa tunaowasikia wakitema cheche, hata hawafafanui msingi na maana hasa ya madai yao, tujichunge nao.
Wanaompinga Pinda, iwe vibarazani, mikutanoni, maofisini na hata katika kumbi kubwa za kuheshimika kama Baraza la Wawakilishi, wangesubiri wanasheria wafanye kazi zao kama Waziri Mkuu alivyoelekeza, wangeonekana wanabembeleza?
Maneno yasiyokuwa na mpangilio baadhi yao yamewabubujika. Badala ya kueleza suala, wanaishia ‘kutukana’, kukejeli, kurusha vijembe, kukebehi na hata kutumia ujuzi wa maneno ya Kiswahili yasiyokuwa na tija yoyote katika ujenzi wa hoja ya suala zima.
Shamuhuna amewahi kukaririwa akiibua hoja tata wakati watu walipokuwa wakisema suluhisho la mpasuko wa kisiasa Zanzibar ni serikali ya mseto. Ilibidi CCM watoe kauli kuwa hayo yalikuwa ni maoni yake binafsi. Lakini kwa hili la sasa, hatujasikia ikisemwa hivyo na chama hicho.
Kutokana na ukimya wa sasa hasa kutoka kwa watu tuliotarajia wawakemee na kuzisukumizia mbali kauli za akina Shamuhuna, tunashawishika kuamini kuwa safari hii kauli hii si ya kwake binafsi, inasukumwa au anasukumwa na wengine wengi nyuma yake.
Na kwa kuwa Shamuhuna si mtu mdogo katika CCM na serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ukiachilia mbali Raza ambaye hatujui alitumia nguvu inayotokana na wadhifa upi kumbeza Tambwe, ukiongeza na ukimya wa ‘mabosi’, tunashindwa pia kujizuia kuamini kuwa huo ndio msimamo atakaokwenda nao katika meza ya majadiliano, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.
Maalim Seif nafikiri katika hili atapaswa kuwaeleza vizuri Watanzania. Kwa sababu mbali na kushangilia hukumu ile kesi ya uhaini ya akina Machano na wenzake mwaka 2000, hivi majuzi kanukuliwa akimsihi Rais Karume atangaze mgogoro wa kikatiba katika Muungano.
Katika mkutano huo wa Kibanda Maiti, kama alivyonukuliwa, Maalim Seif alitumia muda wake akimsifia Mzee Karume, kuwa alikuwa imara asiyepata kuyumbishwa.
Kwa kauli ya namna hiyo tunaweza kusema kuwa Maalim Seif alikuwa akimkubali Karume baba. Lakini wa sasa, hajawahi kutamka hivyo.
Lakini ni Maalim Seif huyo huyo ambaye hajapata kumtambua Karume kama rais wa Zanzibar, kwa misingi ya kwamba alimnyang’anya tonge mdomoni.
Katika hili, ni vyema vyama vyote vinavyosema kuwa vinalilia ‘haki’ au ‘hadhi’ ya Zanzibar viwe na msimamo madhubuti katika makabrasha yao, kama ni katika ilani au katiba zao.
Lakini ili kuonesha kuwa wanarukia mambo, ukitazama katiba zao, itakuwa ni bahati ya mtende kukuta ‘hadhi’ ya Zanzibar imeelezwaje, kama ni dola, nchi, taifa, mkoa, au vyovyote vile. Huko ni kubahatisha mambo.
Sasa CUF imepata changamoto kubwa kutoka kwa mmoja wa wawakilishi wake, aliyeamua kujitolea kumfunga paka kengele.
Bila kutafuna maneno kasema sasa ni muda mwafaka wa chama hicho kuitambua serikali ya Rais Karume. Hakuna haja ya kuendelea kutoitambua serikali kwa muda wote huu na wakati huo huo hali halisi ikionesha kuwa wako pamoja.
Lakini katika harakati zao za kudai nchi yao, ni vizuri baadhi yetu tukaelezwa waziwazi, kuwa ni kipi wanasiasa wetu wanataka kitangulie, kumeguka kwa Muungano au kujitenga kwa Pemba na Unguja.
Kwa sababu kumekuwapo na maneno mengi hasa baada ya kuzorota (au kukwama) kwa mazungumzo ya muafaka kuwa ni bora Pemba akajitegemea, kwani imekuwa ikitengwa katika serikali ya sasa ya Karume.
Sasa hao hao ambao tumepata kuwasikia wakipaza sauti zao wakitaka Pemba iwe na serikali yake, tunawasikia wakitaka Zanzibar isibabaishwe katika Muungano na kwamba inaweza kujitoa. Wana ajenda gani hawa? Kwamba wanajua wakifanikiwa kuuvunja Muungano itakuwa rahisi kwao kukitenganisha kisiwa cha Pemba?
makene_84@yahoo.com 0713 58 44 82
|