MBUNGE wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe (CCM), ameitaka serikali kutoa adhabu kali kwa Naibu Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Ali Juma Shamuhuna na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Ali Pandu Hassan, kwa kuonyesha utovu wa nidhamu kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Mwakyembe alitaka viongozi hao waadhibiwe kutokana na matamshi waliyoyatoa ndani ya Baraza la Wawakilishi hivi karibuni wakipinga kauli ya waziri mkuu kuhusu hadhi ya Zanzibar katika muungano.
Tamko hilo la Mwakyembe ambaye katika siku za hivi karibuni amepata umaarufu mkubwa kutokana na ripoti ya kamati teule aliyoiongoza kuchunguza kashfa ya Richomond, alionya kuwa endapo viongozi hao hawataadhibiwa, basi ipo siku wanaweza kufikia hatua ya kumnyoshea kidole machoni, Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Mwakyembe ambaye alikuwa akizungumza wakati wa kipindi cha maswali ya ana kwa ana kwa waziri mkuu, bungeni mjini Dodoma, alisema kitendo cha mawaziri hao wawili kumpinga hadharani Pinda si tu kwamba ni utovu wa nidhamu, bali pia kinakwenda kinyume cha agizo lake la kuwataka wanasheria wakuu wa muungano na yule wa Zanzibar kulishughulikia suala hilo linalohusu hadhi ya visiwa hivyo katika muungano.
“Kilichotokea Zanzibar kwa viongozi hao ni utovu wa nidhamu na wanapaswa kuadhibiwa na wasipoadhibiwa, kuna siku watamnyoshea kidole rais mpaka machoni,” alisema Mwakyembe na kushangiliwa na wabunge.
Mbali ya kushangiliwa, wabunge wawili, John Malecela (Mtera – CCM), na Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini – Chadema), waliinuka katika viti vyao na kwenda kumpa mkono wa pongezi Mwakyembe mara baada ya kumaliza swali lake.
Katika hali inayoweza kuonyesha kumuunga mkono Mwakyembe, Mbunge wa Muleba Kusini, Wilson Masilingi (CCM), naye alisema suala hilo lililoanzia bungeni, linapaswa kuwa fundisho kwa Watanzania ambao wanapaswa kumwomba Mungu.
Akielezea kile kilichotokea hata kusababisha Pinda kutoa matamshi hayo, Masilingi alisema waziri mkuu alikuwa ndiye aliyechokozwa na mbunge, ingawa yeye ndiye akaanza kuandamwa baadaye.
“Waziri Mkuu alichokozwa na mbunge mmoja, lakini kesi ikawa ya waziri mkuu. Maandamano yameandaliwa kumpinga bila sababu ya msingi,” alisema Masilingi.
Kabla Masilingi hajamaliza kuzungumza, alisimama Mbunge wa Dimani Zanzibar, Hafidh Tahir (CCM), aliyetaka mwongozo wa Spika, akitaka amzuie Masilingi kuendelea na kauli yake, kwa kuwa tayari Spika mwenyewe ameshatamka kuwa suala hilo linashughulikiwa na wabunge waache kuendelea kujadili na kuliuliza bungeni.
Hata hivyo, Spika alimjibu kwa kusema kuwa: “Bado namsikiliza Masilingi anakwenda wapi, lakini kauli yangu isipotoshwe, kama anatoa ufafanuzi wa kikatiba anaruhusiwa,” alisema.
Kauli hiyo ya Spika ilimfanya Masilingi aendelee kuchangia na kusema kuwa waziri mkuu anapaswa kuungwa mkono kwa nguvu zote, kwani yuko sahihi.
Mbunge mwingine wa Kibakwe, George Simbachawene, (CCM), alipotaka kuzungumzia hoja ya Zanzibar ni nchi au la, Spika alimzuia.
Hoja hiyo ya hadhi ya Zanzibar, ilianzia bungeni wakati Waziri Mkuu, Pinda alipokuwa akijibu swali kuhusu nafasi ya Zanzibar, na akajibu kuwa si nchi, akitumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kauli hiyo ilizua malumbano miongoni mwa Wazanzibari wa makundi tofauti ya kisiasa na kijamii, walioungana kutetea hadhi ya Zanzibar kuwa ni nchi, huku wakiungwa mkono na viongozi wao.
Malumbano kuhusu suala hilo sasa hivi yamefikia hatua ya kuwashawishi watu kuanza kutoa lugha za kuashiria mwelekeo mbaya wa muungano uliodumu kwa miaka 44.