Tarishi Hauwawi

August 15, 2008

Varangati la Mahakama ya Kadhi latikisa Bunge

Filed under: habari — tarishi @ 10:44 am

SUALA la Mahakama ya Kadhi limeendelea kurindima bungeni kutokana na mgongano wa msimamo kuhusu suala hilo miongoni mwa wabunge.

Hali hiyo ilijitokeza juzi na jana wakati wabunge hao walipokuwa wakijadili mpango wa maendeleo na makadirio ya matumizi ya fedha ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka huu wa fedha.

Katika utoaji maoni hayo, wabunge ambao ni Wakristo walipinga kuundwa kwa Mahakama hiyo wakisema inaweza kuwa chanzo cha vurugu nchini.

Wabunge Waislamu nao walitetea kwa nguvu uundwaaji wa Mahakama hiyo wakisema wananchi hawana haja ya kuwa na wasiwasi kwa vile itakuwa inashughulikia masuala yanayowahusu Waislamu tu.

Awali, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alipowasilisha makadirio ya Wizara yake, alisema Tume ya Kurekebisha Sheria imekamilisha utafiti kuhusu uundwaji wa Mahakama ya Kadhi nchini na imekwisha kuwasilisha taarifa ya mapendekezo yake serikalini kwa mujibu wa sheria.

“Hivi sasa serikali inaitafakari kabla ya kufanya maamuzi. Bunge litafahamishwa uamuzi wa serikali mara tu utakapotolewa,” alisema.

Katika mjadala huo juzi, aliyekuwa wa kwanza kupinga wazo la kuanzishwa Mahakama hiyo ni Ruth Msafiri- CCM (Muleba Kaskazini) wakati waliotetea wazo hilo ni Athumani Janguo (Kisarawe-CCM), Mohamed Risherd Abdallah (Pangani-CCM) na Mudhihir M. Mudhihir (Mchinga-CCM).

Akipinga wazo hilo, Msafiri alisema suala la Mahakama hiyo likiingia serikalini “tutavurugana”. “Haiwezekani suala la Mahakama ya Kadhi ambalo ni la dini likaingizwa serikalini. Mambo ya dini yamalizwe hukohuko na waumini wa dini husika,” alisema.

Akiunga mkono wazo hilo, Mbunge wa Kisarawe, Janguo alisema suala la kuundwa kwa Mahakama hiyo limechukua muda mrefu na hivyo umefika wakati serikali itoe uamuzi wa kukataa au kukubali.

“Uamuzi ufanywe… uwe mzuri au mbaya, Waislamu waweze kumeza mate,” alisema na kusisitiza kuwa Waislamu bado wanalalamika kwa kutokuundwa kwake.

Risherd alisema Mahakama ya Kadhi itashughulikia Waislamu tu katika masuala ya ndoa, talaka, mirathi na mengine, kugombana na kufikishana Mahakamani na kadhalika; wakati Mudhihir alisema kwa nini Mahakama ya Kadhi inakuwa kikwazo kuundwa upande mwingine wa Muungano ambako ni Tanzania Bara wakati Zanzibar ipo.

Alisema wananchi hawana sababu ya kuwa na hofu kwa sababu ni ya Waislamu tu. Hata hivyo, alitahadharisha: “Mkiwanyima wakianza kulalamika kwa kukosa oksijeni… ikitoka basi ni matatizo.”

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), alisema mjadala huo unaelekea pabaya.

Alisema mtiririko wa uchangiaji wa suala la kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi ambao umechukua nafasi kubwa kujadiliwa kwa siku mbili umeligawa Bunge kwa misingi ya dini.

“Majibizano baina ya wabunge siyo sahihi hata kidogo, tumehama kwenye Bunge la vyama na kuwa Bunge la dini, tuwe wavumilivu na tusikilize maamuzi ya serikali,” alisema Zitto.

Alisema wabunge wamekosa nidhamu na pia wanavunja Katiba ya nchi kwa kuingiza majadiliano kwa misingi ya dini wakati Bunge na Serikali havina dini.

Zitto alisema hakuna anayehitaji kuona Taifa likiparaganyika na kwamba malumbano yanayoendelea hayana msingi kwani hata muswada wenyewe haujaletwa bungeni na kwamba hakuna sababu ya kuishinikiza serikali kuamua suala hilo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe (CCM), alisema michango iliyotolewa na wabunge kwa siku hizo mbili kuhusu suala hilo, inawapa joto wabunge ambalo halina misingi.

Dk. Mwakyembe alisema kuanzishwa kwa Mahakama hiyo hakupaswi kuishinikiza serikali kwa kuwa nchi haiongozwi kwa misingi ya dini na tayari tume imeshalikabidhi serikalini suala hilo kwa maamuzi.

“Kwa kweli mimi nashangaa na nimepata joto la ajabu kuhusu suala hili, sijui wabunge wanafikiri mambo ya uamuzi ni rahisi tu. Hili siyo jambo rahisi tusubiri tuone,” alisisitiza.

Alisema kuanzishwa kwa Mahakama hiyo kupitia serikalini si sahihi kwa kuwa Katiba ya nchi inapinga serikali kujihusisha na masuala ya dini na kwamba hata ikianzishwa ni kodi za Watanzania wote zitatumika kuiendesha.

Mbunge wa Singida Kusini, Mohammed Missanga (CCM), alitahadharisha kuwa isifikiriwe kimakosa kuwa kuunda Mahakama ya Kadhi maana yake ni kuunda Serikali ya Kiislamu. Alisema suala hilo ni la Ibada na akataka wasio Waislamu kuwa wavumilivu na kuzingatia kuwa Waislamu wamevumilia mengi.

Mbunge huyo alitoa mifano kadhaa ya uvumilivu huo aliosema unajumuisha kutolalamika kuhusu Wakristo kupumzika Jumapili siku wanapopaswa kusali na wabunge kukaguliwa magari yao wakati wanaingia bungeni wakati mwingine kwa kutumia mbwa ambaye Waislamu humwona najisi.

Akichangia hoja hiyo Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM), alisema suala la Mahakama ya Kadhi siyo la serikali, bali ni la dini. Alisema ni vyema wabunge wakasoma Katiba na kuielewa hasa kwenye Ibara ya 19 ambayo inaweka bayana suala hilo.

Zambi aliwatahadharisha wabunge wenzake kwa kusema wawe makini kuzungumza mambo yanayohusu imani na kutoyaleta bungeni kwa kuwa kamwe siasa haiwezi kuchanganywa na dini.

Mbunge wa Bukene, Teddy Kasella-Bantu (CCM), alisisitiza hoja hiyo kwa kusema suala hilo liachwe kwenye dini husika na wao ndiyo wenye maamuzi ama ya kuunda chombo hicho au la.

Mbunge wa Muleba Kusini, Wilson Masilingi (CCM) alisema kwa mjadala wa suala hilo, kuna kazi kubwa ya kuliombea Taifa. “Tusijaribu kufunua yale yaliyozibwa bila kufahamu yalizibwaje,” alisema.

Alisema Bunge haliwezi kugawanyika pande mbili kwa misingi ya dini kwa sababu ya malumbano juu ya suala la Mahakama ya Kadhi kwa kuwa serikali imeshapokea taarifa ya Tume inaifanyia kazi.

Awali, Mbunge wa Kigoma Kusini, Manju Msambya (CCM) alisema suala la kuanzishwa Mahakama ya Kadhi ni ahadi iliyo ndani ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alimtaka Waziri kutoa majibu kwa nini Mahakama hiyo ilivunjwa mwaka 1963, na kudai kwamba baada ya kuvunjwa huko, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) lilianzishwa kwa kubambikwa.

Msambya alisema kinachotakiwa ni utekelezaji wa ahadi hiyo ya kurudishwa kwa Mahakama hiyo.

Hata hivyo, Mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes (CCM), alimsihi Waziri Chikawe kusoma hisia za wabunge na kuamua kwa busara suala hilo.

No Comments Yet »

No comments yet.

RSS feed for comments on this post. TrackBack URI

Leave a comment

Blog at WordPress.com.