Tarishi Hauwawi

January 3, 2009

CHADEMA YAPIGWA CHINI MBEYA VIJIJINI

Filed under: habari ndio hiyo — tarishi @ 6:54 am

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetupilia mbali rufani iliyowasilishwa kwake na mgombea wa ubunge kwa tiketi ya Chadema katika Jimbo la Mbeya Vijijini, ambaye ni Mwanasheria wa Kujitegemea, Sambwee Shitambala na kumuengua kutokana na kukiuka taratibu za sheria katika ujazaji wa fomu za uchaguzi.

Akisoma uamuzi wa tume, Mwenyekiti wa NEC Jaji Lewis Makame alikubaliana na pingamizi zilizowekwa na mgombea wa CUF, Daud Mponzi na wa CCM, Mwanjale Luckson, kutokana na mgombea huyo kuapa kwa wakili kinyume cha Sheria Namba 1 mwaka 1985 inayotaka mgombea aape kwa hakimu.

Alisema katika kifungu cha 38 (3) (a) cha Sheria ya Uchaguzi Namba 1 ya mwaka 1985 kimebainisha tamko la kisheria linalotakiwa kufanywa na mgombea ubunge, kuwa hakimu ndiye anayepaswa kushuhudia tamko la kiapo.

“Na katika Sheria ya Tafsiri (Interpretation of Laws Act, CAP I R. E. 2002) na Sheria ya The Magistrate’s Courts of Laws Act’ CAP 11 R. E. 2002) haijumuishi mtu mwingine isipokuwa mahakimu wa Mahakama za Mwanzo, Wilaya na Hakimu Mkazi,” alisema na kuongeza kuwa ni dhahiri wakili hawapaswi kushuhudia tamko husika.

Alisema kwa kuwa tamko limesainiwa na mtu asiyehusika, ni dhahiri tamko hilo sio halali na ni sababu ya kuweka pingamizi iliyotajwa katika kifungu cha 40 (1) (d) cha Sheria ya Uchaguzi ambayo haimruhusu wakili kusaini tamko hilo.

Aidha, alisema sheria za Oaths and Statutory Declaration Act na The Notaries Public and Commissioners for Oaths, ni sheria ambazo zinahusu viapo na matamko ya kisheria kwa ujumla, na kifungu cha 38 (3) (a) kinahusu tamko la kisheria kwa wagombea ubunge tu.

“Kuna kanuni ya sheria inayosema wakati wowote ambapo sheria ya jumla inapoungana na sheria maalumu, sheria maalumu ndiyo inayopaswa kutumika,” alisema Jaji huyo mstaafu.

Alisema kutokana na maelezo ya kifungu cha 38 (3) (a), sheria za viapo haziwezi kutumika katika suala hilo kwa sababu Sheria ya Uchaguzi ya 1985, imetamka bayana kuhusu ni nani anayetakiwa kushuhudia tamko la kisheria la mgombea ubunge na fomu za kutumika katika matamshi hayo zimebainishwa katika kanuni za uchaguzi wa rais na wabunge za mwaka 2005.

“Fomu inataka jina la Hakimu, Saini yake na Muhuri wa Mahakama,” alisema. Kadhalika alisema wagombea walikuwa na muda wa kutosha ambao wangeweza kuwasilisha viapo vyao kwa mahakimu.

“Makatibu wote wa vyama vya siasa ngazi ya wilaya, walipatiwa barua iliyokuwa inaonyesha wagombea wanatakiwa kuchukua fomu kuanzia tarehe 17 mpaka tarehe 27 Desemba siku ya kurudisha fomu na ya uteuzi,” alisema na kuongeza kuwa wagombea walikuwa na siku sita za kazi za kuwasilisha viapo vyao.

Alisema kutokana na maelezo hayo yaliyozingatia hoja tatu za msingi za mrufani, na kwa kuzingatia uamuzi wa NEC katika rufaa ya Ernest Binna, mgombea wa Ubunge Jimbo la Bunda kwa tiketi ya CUF katika Uchaguzi Mkuu wa 2005, Tume ya Taifa inakataa rufaa ya mgombea wa Chadema, mwanasheria Shitambala.

Akizungumza baada ya rufaa yao kutupiliwa mbali na NEC, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Mbunge wa Mpanda Kati, Said Arfi alisema wamepokea uamuzi wa tume na wanahitaji muda wa kutafakari kabla ya kutoa tamko.

“Haya ni maamuzi dhidi ya demokrasia, inawanyima fursa wananchi kuchagua viongozi wao,” alidai Arfi.Wagombea wa vyama vya CUF na CCM viliwasilisha pingamizi dhidi ya mgombea wakiwa na sababu kuu nne likiwamo suala la kiapo ambacho aliapishwa na wakili Evarist Mashiba wa Dar es Salaam, kinyume cha sheria ya uchaguzi.

Uamuzi wa NEC ulifikiwa na majaji wanne akiwamo Jaji Makame; Makamu Mwenyekiti Jaji Omar Makungu; Jaji John Mkwawa na Jaji Mary Longway waliokuwa wajumbe pamoja na Mchanga Mjaka na Hilary Mkate.

Kuenguliwa kwa Chadema kunaacha uwanja wa ushindani kwa vyama vya CCM chenye mgombea Mchungaji Luckson Mwanjale, CUF kikimsimamisha Mhandisi mstaafu Daud Mponzi na mfanyabiashara Subi Mwakipiki kwa tiketi ya SAU.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbarali amekihama chama hicho na kujiunga na CCM kwa madai kuwa ruzuku za chama hicho zimekuwa zikiishia ngazi ya taifa na kuwatelekeza viongozi wa wilaya.

Akizungumza wakati akirudisha kadi ya Chadema katika mkutano wa hadhara wa Chama Cha Mapinduzi uliofanyika wilayani Mbarali juzi, Mwenyekiti huyo Sethi Kitaule alisema ameamua kukihama chama hicho baada ya kuona viongozi wanaothaminiwa na chama hicho ni wa ngazi ya taifa pekee.

Alidai tangu ajiunge na chama hicho, ruzuku zote zimekuwa zikiishia ngazi ya taifa, tofauti na CCM ambayo imekuwa ikipeleka fedha na kulipa mishahara baadhi ya wafanyakazi wake. “Chadema inatukumbuka pale tu uchaguzi unapokaribia, ukipita hatuwaoni tena,” alidai.

Mbali ya Kitaule, zaidi ya wanachama 30 wa vyama vya upinzani akiwamo Burton Kihaka aliyegombea ubunge kati ya mwaka 2000 na 2005, alisema vyama vya upinzani vinaibuka wakati wa uchaguzi tu hivyo kushindwa kuwasaidia wananchi.

Advertisements

Leave a Comment »

No comments yet.

RSS feed for comments on this post. TrackBack URI

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

Blog at WordPress.com.

%d bloggers like this: