Tarishi Hauwawi

January 3, 2009

MGONJA AUNGANISHWA KESI NA YONA, MRAMBA

Filed under: habari ndio hiyo — tarishi @ 7:00 am

Gray Mgonja

Gray Mgonja

Kesi iliyokuwa inamkabili Katibu Mkuu wa zamani wa Hazina, Gray Mgonja, imefutwa jana, badala yake mshitakiwa huyo sasa ameunganishwa katika kesi inayowakabili mawaziri wawili waandamizi wa zamani Basil Mramba na Daniel Yona.

Kutokana na Mgonja kuunganishwa kwenye kesi hiyo ya kutumia vibaya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.7, washitakiwa hao waliomba kurudishiwa sehemu ya mali zao walizowekeza kortini kama dhamana.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam haikuwa na pingamizi na iliamua washitakiwa watakuwa nje kwa dhamana ya Sh bilioni mbili kila mmoja au kuwasilisha hati yenye kiasi hicho cha fedha kutokana na idadi yao kuongezeka.

Awali, Mgonja alikuwa nje kwa dhamana ya Sh bilioni 5.9 kutokana na kushitakiwa peke yake na aliwasilisha hati zenye thamani ya Sh bilioni 6.2. Kwa upande wa Mramba na Yona, walikuwa nje kwa dhamana ya Sh bilioni 2.9.

Kutokana na uamuzi huo, washitakiwa watachagua hati ambazo watapenda kuziondoa mahakamani. Tayari Mgonja ameshaomba aondoe hati ya nyumba ya kitalu 29 iliyoko Adda Estate ya thamani ya Sh bilioni 1.7 na hati ya kitalu namba 80 iliyoko Mikocheni yenye thamani ya Sh bilioni mbili.

Hakimu Mkazi Hezron Mwankenja alisema masharti mengine ya dhamana kama kutoruhusiwa kutoka nje ya Dar es Salaam, kukabidhi hati ya kusafiria kwa waendesha mashitaka na masharti mengineyo yatabaki kama yalivyokuwa awali.

Hatua hiyo ya kuunganishwa Mgonja kulifanya upande wa mashitaka kusoma upya mashitaka kwa washitakiwa wote watatu, huku Mramba akiendelea kukabiliwa na mashitaka yote, Mgonja mashitaka manane na Yona akibakiwa na mashitaka sita.

Hata hivyo, mashitaka yaliyosomwa jana na waendesha mashitaka wa Serikali na wale wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), yamepungua kutoka 13 hadi 12. Kesi hiyo itatajwa tena Februari 2, mwaka huu kutokana na upande wa mashitaka kutokamilisha upelelezi wa shauri hilo.

Katika hatua nyingine, Yona na Mramba wameiandikia barua mahakama kuomba waruhusiwe kusafiri nje ya Dar es Salaam. Yona ameomba siku saba kuanzia leo ili asafiri kwenda kwao Same kuwaona wazazi wake ambao wanaumwa.

Mramba ameomba kusafiri kwenda jimboni kwake kuanzia leo hadi Februari mosi ili kutembelea wapiga kura wake. Pia ameomba aruhusiwe kusafiri kwenda katika vikao vya Bunge Dodoma. Bado hajaruhusiwa uamuzi utatolewa Jumatatu.

Mramba na Yona, wote waliowahi kuongoza wizara nyeti ya Fedha, wanatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yao waliyokuwa nayo kwa kuipendelea Kampuni ya Alex Stewart (Assayers) ya Uingereza kwa kuipa mikataba minono na baadaye kuisamehe kodi.

Mkataba unaotajwa katika kesi hiyo ni wa kukagua hesabu za kampuni zinazochimba dhahabu nchini; bila kufuata sheria za manunuzi ya umma. Baadaye washitakiwa hao wanadaiwa kuiongezea mkataba wa miaka miwili kampuni hiyo bila kufuata taratibu.

Makosa yanayowahusisha vigogo hao wawili ni ya kutumia vibaya madaraka kwa kusaini na kuingia mkataba na kampuni ya ukaguzi wa hesabu kwenye migodi ya dhahabu nchini kinyume cha sheria ya manunuzi.

Kosa hilo la kuingia mkataba na kuiongezea mkataba kinyume cha taratibu wanadaiwa kulifanya kati ya Juni 14, 2005 hadi Juni 23, 2007.

Kosa la tatu pia linawahusu washitakiwa wote watatu ambao wanadaiwa kati ya Machi 2005 na Mei 28, 2005 wakiwa mawaziri walitumia vibaya madaraka yao kwa kuiachia kampuni hiyo kujiongezea mkataba.

Katika shitaka hilo inadaiwa viongozi hao walimwachia Dk. Enrique Segura wa Alex Stewart kukamilisha mkataba wa kujiongezea miaka miwili kabla ya timu ya serikali kufanya majadiliano juu ya suala hilo.

Washitakiwa hao pia wanadaiwa kati ya Machi na Mei 2005 wakiwa mawaziri, waliliachia suala la udhibiti wa madini ya dhahabu kufanywa kienyeji na kampuni hiyo bila kulipeleka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama ilivyoamriwa na timu ya majadiliano ya serikali.

Upande wa mashitaka ulidai kuwa uamuzi wa mawaziri hao uliisababishia Kampuni ya Alex Stewart kuongezewa mkataba wa miaka miwili kabla hata ya suala la ada kuafikiwa na pande zinazohusika pamoja na masuala mengine ya mkataba.

Shitaka la kusababisha hasara ya Sh bilioni 11.7 linawahusu washitakiwa wote watatu ambao wanadaiwa kufanya kosa hilo kati ya Juni 2003 na Mei 28, 2005 wakiwa mawaziri na Katibu Mkuu wa Hazina katika Serikali ya Awamu ya Tatu.

Shitaka la tano linamhusu Mramba na Mgonja wanaoshitakiwa kwa kudharau ushauri uliotolewa na Mamlaka ya Mapato (TRA) wa kuwataka wasiruhusu msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart. Mramba na Mgonja pia wanashitakiwa walitoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume cha ushauri wa TRA.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 10, 2003 na kutoa tangazo la serikali namba 423/2003 la kutoa msamaha wa kodi zote zilizokuwa zinalipwa na kampuni zilizokuwa zinaisambazia vifaa Kampuni ya Alex Sterwart kinyume cha ushauri wa TRA.

Katika kosa lingine Mramba na Mgonja wanashitakiwa kuwa Desemba 19, 2003 wakiwa waajiri wa Wizara ya Fedha walitumia vibaya madaraka yao kwa kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume na ushauri wa TRA.

Oktoba 15, 2004 Mramba na Mgonja pia wanadaiwa waliipa msamaha mwingine wa kodi kampuni hiyo kinyume cha ushauri wa TRA.

Kosa kama hilo Mramba na Mgonja wanadaiwa kulitenda tena kati ya Oktoba 14 na 15 baada ya kutoa tangazo namba 498/2004 la kuruhusu msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart kinyume na ushauri wa TRA.

Katika shitaka la 10 Mramba na Mgonja wanatuhumiwa kutoa msamaha mwingine wa kodi kwa kampuni hiyo. Walitoa msahama huo kupitia tangazo la Serikali namba 377/2005 na kutoa upendeleo huo wa kutolipa kodi kwa kampuni hiyo.

Shitaka la 11 linawahusu Mramba na Mgonja ambao wanadaiwa kutoa msamaha wa kodi kwa Alex Stewart kitendo wanachodaiwa kukifanya Novemba 15, 2005 kupitia Tangazo la Serikali namba 378/2005.

Advertisements

Leave a Comment »

No comments yet.

RSS feed for comments on this post. TrackBack URI

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

Blog at WordPress.com.

%d bloggers like this: