Tarishi Hauwawi

January 3, 2009

SERIKALI YAIKOMBOA ATCL

Filed under: habari — tarishi @ 7:32 am

Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL David Mattaka

Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL David Mattaka

Serikali imetoa Sh bilioni 2.5 kwa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ikiwa ni fedha za awali za kuendesha kampuni hiyo na kulipa baadhi ya madeni kati ya Sh bilioni 3.3 zilizoombwa na kampuni hiyo kama mtaji wa haraka.

Sambamba na hilo, Waziri wa Maendeleo ya Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa ameunda Tume na kuitaka ifanye kazi kwa siku 21 tangu Desemba 29, mwaka jana ili kubainisha kiini cha matatizo ya ATCL baada ya ripoti ya Bodi ya kampuni hiyo kutotoa maelezo ya kutosheleza.

Mwenyekiti wa Tume hiyo ya watu saba ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Profesa Idrissa Mshoro na wajumbe wengine sita, alisema Dk. Kawambwa. Kuhusu mtaji huo wa Sh bilioni 2.5, Dk. Kawambwa aliwaambia waandishi wa habari jana Dar es Salaam kuwa serikali imeamua kuibeba ATCL kuanzia mtaji mpaka ulipaji wa madeni kwa kuwa ni mmiliki wa kampuni hiyo na kwamba itatoa fedha kwa awamu kulingana na mahitaji ya wakati ya kampuni hiyo.

Alisema hapo awali wakati mkataba na Shirika la Ndege la Afrika Kusini unakufa, kulikuwa na deni la takribani Sh bilioni 30 ambazo ni pamoja na Sh bilioni 9.1 za watoa huduma kama ya mafuta ambao ni BP na wasambazaji wa chakula, Sh bilioni saba za uendeshaji na Sh bilioni 17.5 zilizotolewa na serikali kama mkopo.

Alisema deni lingine ni dola za Marekani milioni 4.2 sawa na Sh milioni 5.04 linalodaiwa na SAA ambapo pamoja na kuibeba kampuni hiyo alisisitiza kuwa waliohusika kuihujumu watashughulikiwa ipasavyo, tena mapema.

Alikiri kuwapo matatizo ya utaalamu mdogo katika menejimenti yanayosababisha utendaji mbovu na kusema ni mapema kuchukua uamuzi wa kisiasa kumwajibisha mtu, lakini aliahidi kufanya mkutano karibuni na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya ATCL, Balozi Mustafa Nyang’anyi ili kumpa mwongozo wa namna ya kuchukua hatua za nidhamu kwa waliohusika kuhujumu kampuni.

“Wale ambao watakuwa juu ya uwezo wa Bodi kuwajibishwa, basi Mwenyekiti atapeleka mapendekezo kwa mamlaka ya juu inayohusika ili wawajibishwe na kamwe hatutasita kuchukua hatua zaidi ya hapo kama za kisheria na nyingine kwa wahusika pale itakapobidi,” alisema.

Alisema mbali na madeni hayo ambayo yataendelea kulipwa kwa awamu kulingana na fedha, deni la Sh bilioni 17.5 serikali imelifanya kama mtaji tena kwa kampuni hiyo na pia serikali itatoa Sh milioni 320 kulipa mishahara ya Desemba mwaka jana ya wafanyakazi 300 ambao mpaka leo haijalipwa.

Kuhusu mtaji wa Sh bilioni 91.2 ambao ATCL uliiomba serikali awali, alisema hana kauli kuhusu mtaji huo, lakini alisisitiza kuwa tangu kampuni hiyo iombe mtaji, imenunua ndege mbili aina ya Bombadia, DASH8-Q300 na kukodisha moja, Air Bus 320 kwa gharama za dola za Marekani 370,000 kwa mwezi (Sh milioni 444).

“Lengo ni kuona kampuni yetu inasimama na ndege zinaruka tena, siku za baadaye kuna mpango wa uwekezaji wa mabilioni ya shilingi kwa kununua ndege nyingine, kukodi na kununua vifaa pamoja na kufanya mafunzo…kwa hivyo utaona fedha hizo ni za mahitaji ya dharura ya sasa,” alifafanua Dk. Kawambwa.

Alisema katika hatua hizo zilizochukuliwa na serikali bado mazungumzo yanaendelea baina yake na mwekezaji wa China, ingawa hakuwa tayari kumtaja ila alisema yatakapofikia hatua ya kuridhisha wataweka suala hilo wazi.

Kuhusu ripoti iliyosababisha kuundwa Tume hiyo, alisema kuna mkanganyiko wa maelezo katika taarifa hiyo na mambo kadhaa hajapatiwa majibu hivyo Tume hiyo inapaswa kufuata hadidu tatu za rejea alizozitaja kuwa ni; kubainisha matatizo ya ATCL kitaalamu na kwa kina, kubainisha chanzo chake na kutoa mapendekezo ya mkakati wa kuyatatua na kuhakikisha hayajitokezi wakati mwingine.

Aliwataja wajumbe wengine na wanakotokea katika mabano kuwa ni Dk. Marcellina Chijoriga (Mwenyekiti, Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Profesa Ibrahim Juma (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam), Dk. Gideon Kaunda (Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Kilimo-TCCIA), Mtesigwa Maugo (Shirika la Usimamizi wa Usalama wa Usafiri wa Anga Afrika Mashariki – CASSOA), Dk. Mussa Assad (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) na Dk. Hamisi Kibola (Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji Tanzania-UTT).

Wiki tatu zilizopita Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) iliinyang’anya leseni ATCL kutokana na dosari za kukidhi viwango na kanuni za kiufundi na usalama wa anga. Ilirejeshewa Jumanne wiki hii.

Katika hatua nyingine, serikali imeunda Kamati ya kupitia upya mkataba baina yake na kampuni yenye ubia katika usafiri wa reli ya Rites kutoka India ili kuangalia namna ya kufanya mabadiliko katika Menejimenti ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) baada ya kubainisha kasoro zilizopo katika mkataba huo.

Dk. Kawambwa alisema tayari kikao cha kwanza kimefanyika Novemba mwaka jana na cha pili kinatarajiwa kufanyika siku yoyote katika mwezi huu; lengo ni kuleta uwiano wa kiutendaji katika ngazi mbalimbali za kampuni hiyo kutokana na sasa kuonekana kuwa nafasi kubwa nyingi zinashikwa na wabia wa Rites zaidi.

Advertisements

Leave a Comment »

No comments yet.

RSS feed for comments on this post. TrackBack URI

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

Blog at WordPress.com.

%d bloggers like this: