Tarishi Hauwawi

February 23, 2009

Liyumba, Liyumba, Liyumbaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa!!!!!!

Filed under: habari — tarishi @ 11:07 pm

SIKU moja baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), kutangaza donge nono kwa atakayetoa taarifa za alipojichimbia mshitakiwa wa kwanza, Amatus Liyumba, katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi za umma na kusababisha hasara ya sh bilioni 221, mali ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wananchi mbalimbali wamejitokeza katika taasisi hiyo kutoa taarifa za siri.

Vyanzo vyetu vya habari kutoka katika ofisi hiyo vilisema kuwa licha ya jana kuwa siku ya mapumziko, zaidi ya watu 50 walifika wenyewe katika ofisi hiyo, huku wengine wakipiga simu za kuisaidia TAKUKURU, si tu kwa ajili ya kuhakikisha wanampata Liyumba, bali pia kuibuka na donge nono lililoahidiwa na taasisi hiyo.

“Tunashukuru kwamba wananchi wengi, wameitika mwito, maana hadi kufikia majira ya saa 8:30 mchana, zaidi ya watu 50 walifika kwa siri ofisini kwetu kutoa taarifa za mahala alipo Liyumba.

“Wengine wengi zaidi walitupigia simu na kila taarifa tunaifanyia kazi, tunawaomba wananchi wengine waendelee kutupa taarifa,” alisema mmoja wa maofisa wa TAKUKURU ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.

Huku akiwa makini kuchagua maneno ya kuzungumza, ofisa huyo alisema taarifa hizo zimewasaidia, lakini pia zimewachanganya, kwani ni wachache waliotaja sehemu zinazofanana, huku wengine wakitaja sehemu tofauti za jijini Dar es Salaam, na wengine nje wakitaja mikoa mingine kama Morogoro, Pwani na Arusha, na kusisitiza kuwa taarifa zote wanazifanyia kazi.

Alipoulizwa kwamba haoni kama kinachofanyika kati ya Liyumba na TAKUKURU ni sawa na filamu au mchezo wa kuigiza, ofisa huyo alisema: “Hili ndilo tatizo, maana baadhi wanafikiri ni utani, taasisi yenye dhamana kubwa kama takukuru, haiwezi kujiingiza kwenye usanii wa aina yoyote unaoweza kufikirika.

“Tunasisitiza kuwa kuna donge nono kwa atakayetoa taarifa za kumkatama Liyumba.”

Alisema TAKUKURU inafanya kila iwezalo kumpata Liyumba, kwani kesho anatarajiwa kupanda tena kizimbani ambapo kesi yake inakuja kwa kutajwa kwa mara ya kwanza tangu alipotoka rumande kwa dhamana tata.

Hata hivyo habari zaidi zilisema Liyumba, aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa BoT, anatarajiwa kujitokeza kesho mahakamani baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya hati za mali za sh bilioni 55.

Mbali na Liyumba, mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Meneja Mradi wa BoT, Deogratius Kweka, ambaye hadi sasa bado anasota rumande kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Hatua hiyo ya TAKUKURU kutangaza donge nono kwa atakayetoa taarifa za kumpata Liyumba, zinatokana na juhudi za vyombo vya dola kuanzia Alhamisi ya wiki iliyopita hadi sasa kushindwa kumkamata na kumfikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ambayo Jumatano wiki iliyopita ilitoa hati ya dharura ya kukamatwa mshitakiwa huyo na wadhamini wake wawili.

Wakili wa Serikali, Mwangamilia, ambaye alikuwa akisaidiana na Tabu Mzee kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), alidai mahakamani Ijumaa iliyopita kuwa hawajafanikiwa kumkamata Liyumba kama walivyoamriwa na mahakama hiyo.

Wakili wa mshitakiwa Liyumba, Majura Magafu, ambaye alijiunga rasmi mwishoni mwa wiki iliyopita kumtetea mshitakiwa huyo akisaidiana na Wakili Hudson Ndusyepo, aliiambia mahakama kuwa mteja wake hajafika mahakamani, lakini wadhamini wake ambao ni Otto Agatoni, na Benjamin Ngulugunu walikuwapo mahakamani hapo.

Hakimu Hadija Msongo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alisema kesi hiyo itatajwa Februari 24 mwaka huu (kesho), kama ilivyopangwa awali na kwamba wadhamini hao wanatakiwa kufika siku hiyo pamoja na mshitakiwa.

Hata hivyo, habari ambazo Tanzania Daima imezipata jana kutoka vyanzo vya kuaminika vya habari, zinadai kuwa Liyumba hajatoroka, bali yupo nchini, tena jijini Dar es Salaam, amejificha na anachokifanya ni kuhakikisha anakamilisha masharti ya dhamana, ili kesho atakapofika mahakamani aweze kutimiza masharti hayo.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, taratibu zilizotumika kumpatia dhamana ya awali zitafutwa na atatakiwa aenze upya, hali itakayosababisha kurudishwa tena rumande.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, uvumi ulizagaa jijini Dar es Salaam, kuwa Liyumba ametoroka. Uvumi huo uliifanya mahakama kutoa hati ya kukamatwa kutokana na mazingira ya utata wa dhamana yake, kwani alidhaminiwa kwa hati ya mali ya sh milioni 882, badala ya mali yenye thamani ya sh bilioni 55.

Amatus Liyumba ambaye ametoweka ghafla na kuacha kizaazaa cha aina yake ambacho hakijapata kutokea toka Uhuru

Amatus Liyumba ambaye ametoweka ghafla na kuacha kizaazaa cha aina yake ambacho hakijapata kutokea toka Uhuru

Liyumba na Kweka wanakabiliwa na matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuidhinisha ujenzi wa minara pacha ya BoT, maarufu kama ‘Twin Towers’ na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Advertisements

1 Comment »

  1. Just passing by.Btw, you website have great content!

    _________________________________
    Making Money $150 An Hour

    Comment by Mike — March 1, 2009 @ 8:59 am | Reply


RSS feed for comments on this post. TrackBack URI

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

Blog at WordPress.com.

%d bloggers like this: